Katibu tawala wa Mkoa wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega,
amesema utapiamlo sasa basi kwa mkoa wa Arusha, kwa kuwa wakulima na walaji wa mbogamboga wameungana
pamoja kwa lengo la kuhimiza ulaji mzuri wa mbogamboga.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua warsha ya siku moja
ya wadau wa uzalishaji na ulaji wa mbogamboga katika halmashauri ya Jiji la
Arusha,halmashauri ya Arusha na halmashauri ya Meru.
Kwitega amesema, lishe ina muunganiko wa uzalishaji na
uwandaaji wa vyakula tunavyotumia kila siku katika maisha ya mwanadamu.
Hata hivyo amesema,mpango wa kutokomeza utapiamlo kwa
mkoa wa Arusha umelenga hasa kwa makundi matatu maalumu; Watoto,Wagonjwa,Wanawake
walio katika umri wa kuzaa na Wazee.
Kwitega amesisitiza zaidi kuwa utapiamlo unasababishwa
na upungufu wa Wanga, Vitamin, Madini,Unene kupita kiasi na wathirika wakubwa
ni watoto wenye umri chini ya miaka 5 na wanawake walio katika umri wa kuzaa.
Mbali na hayo amesema changamoto kubwa zinazosababisha
hali ya utapiamlo kuongezeka katika Mkoa wa Arusha ni pamoja na hali ya
umaskini kwa jamii,ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii.
Pia utashi na uwajibikaji wa baadhi ya viongozi,
wananchi kuwa tegemezi na mabadiliko ya tabia nchi.
Hivyo elimu sahihi kwa wananchi itasaidia kutokomeza
kabisa tatizo la utapiamlo na kupelekea kuwa na kizazi chenye afya bora na
kuweza kukuza uchumi wa nchi kwani uzalishaji nao utakuwa.
Mganga mkuu wa Mkoa Wedson Sichalwe amesema, jitihada za
pamoja bado zinaitajika kati ya serikali, wadau na wananchi katika kuhakikisha
utapiamlo unatokomezwa kabisa katika mkoa wa Arusha.
Sichalwe amesema kama Mkoa utaendelea kushirikiana kwa
karibu sana na wadau na wakulima wa mbogamboga katika kuhakikisha elimu sahihi
inawafikiwa walaji na hata wakulima wenyewe juu ya uzalishaji na ulaji wa
mbogamboga.
Akisoma taarifa fupi ya mradi wa uzalishaji na ulaji mbogamboga
Mratibu wa Mradi bwana Peter Bayo kutoka taasis ya ANGONET amesema, mradi huo
kwa kuanzia utakuwa katika halmashauri ya Jiji la Arusha, halmashauri ya Arusha
na halmshauri ya Meru.
Amesema takribani 93% ya wananchi hawatumii mbogamboga
katika milo yao na hali hii kupelekea kiwango cha utapiamlo kuwa juu.
Mradi huo unatarajia kuwafikia takribani watu 1000 kila
wilaya na hasa kwa wakulima wenyewe wa mbogamboga na wanafunzi katika shule za
msingi kwa kuwafundisha kuanzisha vitalu vya mbogomboga katika maeneo ya shule
zao.
Peter amesema, mradi huo una miezi 3 tokea kuanzishwa na
takribani kata 3 za kila wilaya zitahusishwa na mradi huu na wanatarajia zaidi
ya wakulima 3000 watanufaika nao.
Amesema mradi huu wa uzalishaji na ulaji wa mbogomboga
utahusisha zaidi utoaji elimu sahihi ya lishe na ulaji wa mbogamboga, kuanzisha
bustani za mbogamboga katika mashule,watafanya warsha mbalimbali za
uhamasishaji,utayarishaji na upikaji bora wa mbogamboga.
Mradi wa uzalishaji na ulaji wa mbogamboga umeanzishwa
rasmi katika Mkoa wa Arusha na taasis ya ANGONET,TAHA na RULIDE & COMECA kwa kushirikiana na
serikali ya Mkoa wa Arusha ili kuimarisha hali ya lishe na kutokomeza
utapiamlo.
